-
Taifa La Waswahili -
Muhammad bin Yusuf.
-
Madhehebu ya Lugha ya
kiswahili - Ali Said Sunkar.
Taifa La
Waswahili - Muhammad bin Yusuf.

Swahili ni
Taifa la makabila yaliopo katika Pwani ya Afrika ya
Mashariki na visiwa vyake tokea Barawa hadi Sofala. Baadhi
ya makabila hayo ni Wabarawa, Wapate, Waamu, Wagiriama,
Wadigo, Waduruma, Wakauma, Wakambe, Wachoni, Warabai, Waribe,
Wajibana, Wakilindini, Wajomvu, Wamtwapa, Wachangamwe,
Watangana, Wamvita, Wapokomo, Wavanga, Wamakunduchi, Wapemba
na Wangazija. Kabila hizi zote zilikuwa zikizungumza lugha
ilokuwa ikijulikana kama Kingozi. Hata hivyo, makabila yote
haya yalikuwa na ndimi (dialect) zao na miji yao; baadhi yao
bado wangali na ndimi zao na miji yao. Ndimi zote hizi zina
ukhusiano au ukuruba mkubwa wa maneno na maana zake. Kwa
mfano, utakuta kwamba kuna ukuruba fulani baina ya Kipemba
na Kiamu.
Kila kabila ina ndimi yake, dasturi zake, mila zake, tungo
zake, na kadhalika. Haya yote ni kabla ya Waarabu na
Washirazi hawajaanza kuhamia kimaisha katika Pwani ya Afrika
ya Mashariki - takriba karne nane hadi kumi zilizopita (yaani
baina ya miaka 800 hadi 1000).
Washirazi hawakuathiri mno mila, dasturi, mapisi, na lugha
hiyo ya Watu wa Pwani. Waarabu ndiyo walioathiri sana,
khususa Makabila ya Kati na Kati (kwa mfano, Wamvita,
Watangana na Wakilindini). Makabila haya yaliathirika mno
hadi ya kuwa majina haya yalipotea na ndimi zao za kiasili
zilipotea vilevile. Ndimi ambazo bado zipo ingawa zimeazima
maneno fulani ya Kiarabu (kama ambavyo pengine Kiarabu
kimeazima kutoka Lugha ya Kingozi) ni ndimi za kaskazini na
zile za kusini.
Ndimi za Kaskazini ambazo bado zipo na wenyewe wanatambuliwa
ni kama vile Kibarawa, Kiamu, Kipokomo, na kadhalika. Ama
Ndimi za Kusini ambazo hazikuathiriwa mno ni Kingazija,
Kimakunduchi, Kipemba na Kivanga. Ndimi za Kati na Kati
ambazo bado zikalipo ni kama vile, Kigiriama, Kiduruma,
Kijibana; hizi ni miongoni mwa kabila ambazo leo zajiita au
zatambuliwa kama Mijikenda (yaani miji tisia).
Utakuta ya kuwa katika makabila ya kati na kati, yale ambayo
hayakuathiriwa sana ni yale ambamo watu wake hawakuwa
Waislamu. Na ndiyo maana mpaka hii leo utaona ya kuwa
makabila ya Mijikenda (isipokuwa Digo), ni makabila ambayo
wengi katika watu wake si Waislamu. Hii ni kwa sababu
makabila kama ya Mvita, Tangana na Changamwe hayakujitahidi
au kujishughulisha kufanya usambazaji wa Risala ya U-Islam
kwa makabila haya; Waarabu piya walipokuja hawakuwa na lengo
hilo la kuingia vijijini kufanya Da’wah. Lengo lao kubwa
ilikuwa ni biashara. Kama tujuavyo U-Islam ulifika Kaskazini
Mashariki mwa Bara la Afrika kabla haujafika katika sehemu
nyengine za bara Arabu kama vile, Yemen, Omani na hata
katika mji wa Madina na sehemu nyingi za nchi tunayoijua leo
kama Saudi Arabia. Yaani U-Islam ulifika Abisinia (Ethiopia
ya leo) katika mwaka wa 615, miaka mitano tu baada ya Mtume
Muhammad (s.a.w.) kupewa risala (610). Mtume alizaliwa mwaka
wa 570. Ingawa wale Waislamu waliokuja kuomba hifadhi
Abisinia walikwenda zao Madina baada ya kutawazwa kwa
serikali ya kwanza ya Islam mwaka wa 623 (huu ni mwaka wa
kwanza wa Hijria), walikuwa washawasilimisha watu kadha wa
kadha (akiwemo Mfalme wao, Najash); hii ndiyo ilikuwa ni
sababu ya kuanza kusambaa kwa U-Islam katika bara la Afrika.
Kwa hivyo ni muhimu kutambua na kuamini ya kuwa makabila
fulani ya Afrika ya Mashariki yalisilimu kabla ya kuja kwa
Waarabu hawa tuwajuwao leo, waliokuja kwa biashara katika
pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Yemen, Omani, na
kadhalika.
Na khususa ni Waarabu hao wa Yemen na Omani ndiyo waloowana
na baadhi ya hao Wangozi, au wanaojulikana leo kama
Waswahili. Kwa hivyo, baadhi ya Waswahili wana damu za
Kiarabu na baadhi yao hawana damu ya Kiarabu. Katika dasturi
za Kizungu za kufuata ukoo, mtu anapotanganya tu damu na
asekuwa Mzungu, basi azaliwae katika mtanganyiko huo katu
hakubaliwi kuwa ni Mzungu. Na ndiyo twaona ya kuwa ingawa
kuna asili mia thalathini (30%) ya Wamarekani Weuse
(African-Americans) ndani ya Marekani, lakini wanasibishwa
na U-Afrika na U-weuse (Blacks) pekee, na katu
hawanasibishwi na uzungu. Kwa Waarabu nao ni rahisi zaidi
kunasibishwa na taifa hilo ikiwa mtu lugha yake ya kwanza ni
Kiarabu. Ama kwa Waswahili tukati na kati, yaani aghlabu mtu
hunasibishwa na Uswahili kwa lugha na asili. Kwa hivyo leo
wako baadhi ya Waswahili wenye damu za Kiarabu ambao
wametagua, kwa sababu mbalimbali, kujinasibisha zaidi na U-Arabu
kuliko U-Afrika; kadhalika, kuna baadhi yao, kwa sababu moja
au nyengine, wameamua kujinasibisha zaidi na U-Afrika kuliko
U-Arabu.
Hakuna yoyote atakayekataa ya kuwa neno Swahili au Sawahel
ni neno lenye asili ya Kiarabu, ambalo lina maana ya Pwani
au Mwambao. Kwa hivyo, ni wazi kabisa kuwa jina au neno
Swahili halikuapo kabla ya kuja kwa Waarabu. Hivyo basi,
wema mmoja ambao Waarabu waliwafanyia wenyeji wa Mwambao wa
Afrika ya Mashariki na visiwa vyake ni kuwabandikiza neno
lililoanza kutumika kama jina la taifa la wenyeji hao,
litambulikanalo leo hii kama Taifa La wa-Swahili, yaani
Taifa La wa-Mwambao. Watu wa taifa hili ni Waswahili, yaani
Wamwambao, au kwa jina la kiasili, Wangozi. Na hapo pao napo
paitwa Uswahilini. Na mila na dasturi zao ndiyo Uswahili. Na
lugha ya watu hawa ni Kiswahili. Ni lugha ambayo maneno yake
zaidi yatokamana na ndimi za makabila ya kati - kama vile
Kimvita, Kichangamwe na Kitangana; halafu ikatukua na maneno
ya Kiamu, Kivanga, Kipemba, Kingazija, Kibarawa, Kigiriama,
na kadhalika. Kwa hivyo, Kiswahili ni kile kile Kingozi,
tofauti ni jina tu; timbuko lake ni mtanganyiko wa ndimi za
makabila ya Pwani. Piya kuna maneno ya Kiarabu, Kishirazi,
Kiingereza, Kireno, na lugha za bara ya Afrika ya Mashariki.
Kiswahili kimeazima maneno ya lugha nyegine kama ambavyo
lugha zote zimefanya hivyo. Wao na Wahindi piya wameazimiana
katika Upishi. Yayumkinika kuwa katika Kireno, Kiarabu na
lugha nyenginezo kuna maneno ya Kimvita, Kijomvu, Kiamu, na
kadhalika. Hili ni suala ambalo halihitaji mjadala mkubwa
kwani liko waziwazi. Ikiwa baba Adamu (a.s.) na mama Hawaa
walizungumza lugha moja kwa nini leo tuwe na lugha, makabila
na mataifa tungu nzima? Tazama katika Quraani [Al-Hujuraat
aya 13 na Ar-Rum aya 22].
Kwa mfano ukiangalia namna mataifa ya Arabu na Yahudi
yalivyoanza utaona ya kuwa ni kama mtezo. Historia na dini
yatueleza kuwa Mayahudi na Waarabu wanatokamana na Mtume
Yaaqub (a.s.) na Mtume Ismael (a.s.). Ikiwa hii ni kweli,
kwa nini iwe hivi na wote wawili wanatokana na Mtume Ibrahim
(a.s.) ambae taifa lake hatulijui wala hatukuelezwa. Kwa
nini wajukuu, vitukuu, vilembwe, na vilembwekeza vya Nabii
Ibrahim wawe na taifa tofauti na yeye? Tena tofauti yenyewe
si ya taifa moja bali mataifa mawili, angalau!
Mwana Ismael azae Waarabu na mjukuu Yaaqub (mtoto wa Is-haka)
azae Mayahudi. Hii yote hapa ni kuwa tunajaribu kuonyesha ya
kuwa kunahitajika sababu ndogo mno (pengine hata isiyoingia
akilini mwetu) kuzaliwa kwa taifa jipya au kabila mpya.
Lakini hii ni kazi ya Allah (s.w.t.) kama aya za hapo juu
zinavyoonyesha. Halafu isitoshe, baada ya kuzaliwa kwa Taifa
la Arabu, kukaanza Makabila kama vile Qureish, Aws, Khazraj,
na kadhalika. Bado haijatosha, kukazaliwa Koo mbali mbali,
kama vile kwenye kabila ya Qureish kuna koo kama Umayya,
Makhzum, Alawi, Hashim na kadhalika. Ikiwa haya yote
yawezekana, kwa nini visiwezekani kuapo kwa taifa la Swahili
na makabila kama vile Mvita, Ngazija, Giriama, na Makunduchi?
Au kwa nini kusiwe na koo kama vile Mwinjaa, Wanyali,
Wamuyaka, na kadhalika?
Hii leo ni jambo gani linalomuunganisha Muarabu kutoka Sudan
na yule wa kutoka Lebanon na yule wa kutoka Hijaz? Sio dini,
wala rangi, wala nywele, wala tabia, wala mapishi! Huenda
moja au zaidi ya mambo haya yakafanana, lakini jambo kubwa
linalowafanya wote wakaitwa Waarabu ni Lugha, na labuda
Asili. Labuda na Mayahudi ni vile vile, mtukue Yahudi wa
Palestine, na yule wa Habashi na yule wa Urusi; kitu
kitakacho waunganisha ni Asili, na pengine lugha na dini.
Kwa hivyo Swahili ni taifa ambalo lipo, na lenye makabila
yasiopungua kumi na tano, tokea mji wa Barawa (kaskazini)
mpaka mji wa Sofala (kusini). Ni taifa ambalo makabila yake
yametapakaa katika nchi sita: Somalia, Kenya, Tanganyika,
Zanzibar, Ngazija (Comoro Islands), na Msumbiji
(Mozambique). Kwa hiyo, nasema tena ya kuwa Swahili ni Taifa.
Ni muhimu kufahamu ya kuwa mtu anaposema kuwa yeye ni
Mswahili haimaanishi kuwa kabila yake ni Swahili bali ni
kuwa anatokamana na Taifa La Waswahili. Na kitu
kinachowaunganisha watu katika taifa hili ni: Asili na Lugha.
KWAHERINI
Muhammad bin Yusuf
Chapa ya mara ya kwanza - Mwezi wa Ramadhan, 1415 Hijria
(1995)
Madhehebu ya
Lugha ya kiswahili - Ali Said Sunkar.

Kwa mtazamo
wa haraka lakini wa ndani kidogo, tunapotafiti uzungumzi wa
lugha ya Kiswahili hivi leo, tutapata kuwa, kuna Madhehebu
matatu makubwa ambapo Waswahili wote na wazungumzi wa
Kiswahili, wanaangukiya katika mojawapo ya madhehebu haya
matatu.
Na kwa mara nyingine utamkuta mtu akitumiya na kuchanganya
madhehebu mawili au yote matatu pindi anapoongeya au
anapoandika, bila yeye kutambuwa ni mfuwasi au mtetezi wa
dhehebu lipi.
Katika makala haya mafupi, tutajaribu kuangaliya kiini na
chanzo cha kila dhehebu, watetezi wao, wafuwasi wao, uzuri
na ubaya wa kila dhehebu na mwisho itafuatiwa na mapendekezo.
Madhehebu yenyewe ni kama yafuwatavyo:
1) Dhehebu la kwanza hapa nitaliita: "Kiswahili Lahaja yetu"
2) Dhehebu la pili: "Kiswahili Sanifu"
3) Dhehebu la tatu: "Kiswahili Asiliya".
UCHAMBUZI WA MADHEHEBU MATATU
Sasa tuchambuwe nukta zilizotanguliya moja baada ya nyingine
katika kila dhehebu.
DHEHEBU LA KWANZA
1) "Kiswahili Lahaja yetu" inakusudiwa" ule uzungumzi au
uwandishi wa lugha ya Kiswahili unaotegemeya lahaja moja
maalum (makhsusi) miongoni mwa lahaja 23 za Kiswahili
zinzotambulikanwa, kama: Kiamu, Kibajuni, Kibarawa,
Kingazija, Kimvita, Kiunguja na kadhalika.
Kwa miyaka mingi sana utumiyaji wa Kiswahili ulitegemeya
dhehebu hili, hivi kwamba vitabu makhtuti (nyaraka za zamani
au ‘manuscripts’) ambazo ziliandikwa kuanziya karne ya nane
(Eighth century C.E.) hadi karne ya kumi na tisa (19 th
century C.E), zilitumiya lahaja makhsusi ya yule mwandishi
au lahaja ya pale mjini alipo yule mwandishi.
Makhtuti kama hizi zilihifadhiwa kwa njiya mbali mbali
katika mwambao wa pwani, kuanziya Barawa hadi Sofala na
visiwa vya Bahari ya Hindi. Kwa mfano vitabu vilivoandikwa
Amu au vilivyoandikwa na Waamu, utakuta kuwa vilitumiya
Lahaja ya "Kiamu" na vile vilivyoandikwa Mombasa (Mvita),
vilitumiya Lahaja ya "Kimvita" na hivyo hivyo vya unguja,
Pemba na kwengineko.
Itakuwa ni vizuri hapa kugusiya kuwa Ndaki (Vyuo vikuu)
kadhaa za Ujerumani na Uingereza zimejishughulisha sana kwa
muda mrefu tangu karne ya kumi na nane kukusanya na
kuhifadhi hizo Makhtuti. Ambapo hivi leo wamejilumbukiziya
maelfu ya Makhtuti kama hizo kwenye zahanati za kuhifadhiya
makhtuti na nyaraka za zamani.
Miaka kadhaa (80s & 90s) iliyopita wenye Makhtuti kama hizo
Lamu, Malindi, Mombasa, Zanzibar, Tanga na miji mingine ya
Waswahili, walilipwa karibu Shilingi elfu kumi na tano (Ksh
15,000) kwa kila makhtuti moja mtu akionyesha na wajerumani
wachukuwe nakala (photocopy) yake.
Kwa bahati, makhtuti zote walizozikusanya zilikuwa
zimeandikwa kwa kutumiya herufi za Kiarabu, kwa hivyo kazi
nyingine iliyofanywa na Wajerumani na Waingereza, ilikuwa ni
kutafuta wataalamu wa Kiswahili wa Lahaja mbali mbali na
wenye uzoefu wa kufahamu maandishi ya Kiarabu, ili
wazifafanuwe katika herufi za Kilatini na kadhalika
kutafsiri maneno ya kizamani ambayo kwa sasa aidha
hayatumiki au hayaeleweki na watu wa kawaida.
Prof. Ahmad Nabhany ni mmoja wa wataalamu waliofanya kazi
hizo. Ametumiya miaka mingi akitembeleya Ndaki kadhaa za
Ujerumani, Uingereza Afrika Mashariki na Marekani akihadhiri
(Lecturing) juu ya lugha ya Kiswahili.
Kwa hivyo “Kiswahili Lahaja yetu” ilkuwa ni utumiyaji wa
Kiswahili uliotegemeya Lahaja moja au nyingine, kulingana na
mwandishi ni mtumiyaji wa Lahja gani, au yuko mji gani. Na
tukizingatiya njiya nzito za mawasiliano za wakati huo ndio
utaona kuwa ilikuwa sirahisi kwa Waswahili wa kawaida kujuwa
tofauti ya Lahaja hizo, ila wale wataalamu
waliojishughulisha na masuala ya Kiswahili, fasihi, hadithi
ngano (hadithi ndefu) tunzo, mashairi na nyanja
nyingine za lugha ya Kiswahili.
DHEHEBU LA PILI
2) “Kiswahili Sanifu”: dhehebu hili lilianza kuundwa kati wa
karne ya kumi na tisa na karne ya ishirini. Sababu ya
kuundwa dhehebu kama hili ni ile haja ilyokuwepo ya watu (Waswahili)
wote kutoka Lahaja mbali mbali waweze kukutana na waelewane
katika uzungumzi au utumiyaji wa Kiswahii ambao utakuwa ni
sahali kwa wote.
Fikra hii iliungwa mkono na wataalamu wengi wa Kiswahili na
ikaanza kusambaa. Ndiyo wakati huu huu piya, Wanamisheni
(Christian Missionaries) waliokuwa na hamu kubwa kusambaza
ukiristo miongoni mwa Waswahili, na kufunguwa njiya kwa
wakoloni kuingiya Kenya, kama ilivyokuwa kawaida ya wakoloni
kabla ya kuja wao mwanzo hutuma wanamisheni kufunguwa mlango
kwa jina la yesu kristo, walichangiya katika usambazaji wa
Kiswahili.
Wanamisheni wenyewe walikuwa ni wageni katika lahaja yoyote
ile ya Kiswahili. Kwa hivyo waliona kuwa wakilemeya upande
mmoja watakosa wafuwasi wa pande nyingine, basi nao wakaunga
mkono fikra kama hii. Na kwa kuwa wao walikuwa na uwezo
mkubwa wa kifedha na kitaaluma mbali mbali, basi waliweza
kwa muda mfupi sana kubuni uwandishi wa Kiswahili kwa
kutumiya dhehebu hili jipya la “Sanifu”.
Kiswahili ilikuwa ndiyo lugha ya biashara, elimu, utamu wa
fasihi, hisiya za ndani (emotions),mawasiliano ya rahisi.
Kadhalika ni lugha ya utajiri wa maneno ikilinganishwa na
lugha nyinginezo za eneo hilo la Afrika mashariki na kati,
na juu ya yote ilikuwa ni lugha yenye uwezo na fursa ya
kupanuka zaidi na kusambaa sehemu nyingi.
Vitabu vingi vikaanza kuandikwa, ambapo lengo kubwa kwa
upande wa wanamisheni ilikuwa ni kutafsiri Bibliya kwa lugha
ya Kiswahili, hasa baada ya kuona kuwa Kiswahili ilikuwa ni
lugha inayoeneya kwa haraka na kuzungumzwa na watu wengi
sana, hata wale wasiokuwa Waswahili, walipendeleya kutumiya
Kiswahili.
Makamusi ya Kiswahili yakachapishwa, Mashule yaliokuwa
tayari yameshaanzishwa na wanamisheni yakaingiza lugha ya
Kiswahili katika Manhaji (Curriculum) zao, na vitabu vya
shule vya Kiswahili (text books) vikatayarishwa. Matangazo
ya Mongoya (radio) ya wanamisheni na serikali ya kikoloni ya
Afrika Mashariki (East Africa Protectorate), yalizidi
kutiliya nguvu usambazaji wa lugha ya Kiswahili.
Jambo muhimu la kutaamali kidogo ni kuwa, wakati wa
usambazaji wa Kiswahili “Sanifu”, Lahaja mbili pekee (
Kimvita na Kiunguja) ndizo zilizozingatiwa. Ama Lahaja
nyingine ziliachwa nyuma. Jambo hili limesababisha vizazi
vilivyokuja baadaye wakawa hawajui kuhusu hizo Lahaja
nyingine, hali hii imeendeleya kudhuufisha mpaka watu wa
Lahaja yao kuanza kuacha Lahaja na kuisahau na badala yake
wakitumiya “Sanifu”. Kwa hakika Lahaja mbili hizi
zilichaguliwa si kwa sababu ni mzuri zaidi kuliko nyenginezo,
au Lahaja hizo
nyengine ni mbaya, hasha, bali ni kwa sababu Lahaja hizi
zilikuwa katika makao ya utawala, yaani Zanzibar na Mombasa.
Na siku zote makao ya utawala kila mahali ndio yenye
taathiri (influence) kubwa zaidi kwa sababu ya vifaa mabali
mbali (tools and means of communications) zinazomilikiwa na
serikali kwenye makao ya utawala.
DHEHEBU LA TATU
3) “Kiswahili Asiliya” Hili ni dhehebu jipya zaidi kwa
upande mmoja na si jipya kwa upande mwingine. Ni jipya kwa
kuwa watetezi wa dhehebu hili wamekuja na mtazamo mpya wa
utumiyaji wa Kiswahili na kupinga mtazamo wa utumiaji
Kiswahili “Sanifu”.
Ama si jipya ni kwa kuwa watetezi wa dhehebu hili
wanapiganiya utumiyaji wa Kiswahili kwa Lahaja zote ikiwemo
lahaja za Kimvita na Kiunguja. Kwa maoni yao ni kwamba
lahaja zote ni lazima zichanganywe ili ziunde Kiswahili
kimoja chenye utajiri wa maneno wa lahaja zote, na hivi ndio
kurudi katika asili ya Kiswahili, hii ndiyo maana dhehebu
hili linaitwa “Kiswahili Asiliya”
Kwa hivyo “Kiswahili Asiliya” tukitizama kwa makini tutaona
kuwa si jambo geni hivyo, bali ni harakati ya usahihishaji
(Reform Movement) ya ule mtazamo uliosababisha kubuniwa kwa
dhehebu la “Sanifu”, la kutegemeya lahaja mbili pekee. “Asiliya”,
badala yake inapiganiya utumiyaji wa Kiswahili ambao
utashirikisha Waswahili (au wazungumzi wa Kiswahili) wa
lahaja (ndimi) zote.
Lakini kosa au kasoro iliyofanywa na “Sanifu” ni kwamba
mwishowe waliangukiya kutumiya lahaja mbili pekee na kuwacha
nyuma au kutupiliya mbali lahaja nyengine. Na “Asiliya” hivi
sasa inajaribu kurekebisha kosa hilo. Kwa sababu kulingana
na hoja ya watetezi wa “Asiliya” ni kwamba:
utumiyaji wa “Sanifu” wa lahaja mbili pekee, unanyima lugha
ya Kiswahili ule utamu wake ambao unapatikana katika lahaja
nyengine. Vile vile kuna maneno mengine ambayo hayapatikani
katika lahaja za Mvita na Unguja, lakini yanapatikana katika
lahaja nyengine. Kwa hivyo utajiri wa Kiswahili utakamilika
tu pale lahaja zote zitakaposhirikiyana na kutumika sambamba,
hii ndiyo “Asiliya”
Na hivi leo watetezi na wafuwasi wa “Asiliya” wanazidi
kuongezeka, na "Asiliya” yenyewe inaanza kukubaliwa na
wataalamu wengi wa Kiswahili katika Ndaki mbali mbali za
Kenya, Tanzania, Uganda, Ujerumani, Uingereza, Marekani na
kwengineko.....